Sheria mbali mbali zinazo zungumzia
makosa ya jinai hutaja adhabu ambazo mtu anapaswa kupata kutokana na makosa
hayo. Adhabu hizi huweza kuwa faini, kifungo, fidia au vyote kwa pamoja.
Endapo mtuhumiwa atakutwa na hatia
ya makosa hayo Mheshimiwa hakimu/Jaji anatakiwa kuzingatia sheria inayotoa adhabu
hizo pamoja na sheria ya kima cha chini cha
hukumu[1]
inaelezaje, bila kusahau baadhi ya kanuni kutoka katika kesi zilizo kwisha
amuliwa.
Pindi Mtuhumiwa anapopatikana na
hatia Mahakama hutoa nafasi kwa muendesha mashtaka kueleza kwa nini Mtuhumiwa
apewe adhabu inayostahili kama sheria inavyotaka na pia mahakama itatoa nafasi
kwa mtuhumiwa aliyekutwa na hatia kuiomba Mahakama impunguzie adhabu na kwa
sababu zipi.
Kifungu cha sita cha sheria ya kima cha chini cha hukumu kinatoa
ruhusa kwa Mahakama kutoa hukumu kwa Mtuhumiwa aliyehukumiwa kwa mara ya kwanza
kuhukumiwa kanakwamba sheria hiyo haipo, yani kuhukumu vile itakavyoona inafaa.
Kanuni ambazo mahakama inapaswa kuzingatia
katika kutoa hukumu zinainishwa katika kesi ya Jamuhuri dhidi Kidato Abdullah[2]
ambazo ni uzito wa kosa hilo, rekodi
ya mtuhumiwa, umri, maslahi ya jamii ukilinganisha na maslahi ya mtuhumiwa.
Katika kesi ya Jamuhuri dhidi ya Asia Salum na wengine[3] Jaji Mnzavas alibadili adhabu ya mama na
mwanae ambao walikutwa na hatia ya kumpiga mlalamikaji mpaka kumvunja bega la
kushoto na kumuumiza usoni hivyo kuhukumiwa miezi kumi na mbili jela, huku
adhabu halisi ikiwa ni miaka mitano.
Katika kesi hii Jaji alizingatia
kuwa mtoto alikuwa na umri wa miaka 16, alikuwa kidato cha tatu na lilikuwa
kosa la kwanza hivyo alimuachia huru akisema kuwa muda aliokuwa amekwisha kaa
jela umetosha kama adhabu.
Kwa upande wa mama, Jaji alimuhukumu
miezi mitatu badala ya kumi na mbili jela kwa sababu lilikuwa kosa lake la
kwanza na hakuwa mkorofi kaika jamii.
Pia katika kesi hii Jji alisema vitu
viwili vikuu vya kuzingatia, nanukuu;-
(i)
Pale ambapo mtuhumiwa amekutwa na hatia kwa mara
ya kwanza basi mkazo uwekwe katika adhabu ya kumbadilisha, labda tu kosa liwe
kubwa kiasi cha kuhitaji kutoa adhabu ya
fundisho au kosa liwe limeenea sana kiasi cha kuhitaji kutoa adhabu ya kuitisha
jamii,
(ii)
Mtuhumiwa aliyekutwa na hatia kwa mara ya kwanza
hapaswi kupelekwa gerezani ambapo anaweza kujichanganya na wahalifu sugu wa
misimu ambao wanaweza mfundisha kuwa muhalifu.
Lakini pia katika Kesi ya Jamuhuri dhidi ya Kabula Mhoja[4]
Mahakama kuu ilimuongezea adhabu ya mwaka mmoja jela, Kabula aliyehukumiwa na
mahakama ya chini kifungo cha miaka minne
Katika kesi hii Kabula alivunja
mikono ya mtoto wa miezi minne kwa kutumia mikono yake. Kabula hakubahatika
kupata mtoto kutoka kwa mme wake ambaye alizaa nje ya ndoa na mwanamke
mwingine. Hivyo kutokana na kejili za mme wake, kabula siku ya tukio
alimtembelea mke mdogo wa mme wake nakuomba kumuona mtoto, alipokabidhiwa mtoto
ndipo Kabula alivunja mikono ya mtoto huyo.
Kwa kuzingatia uzito wa kosa
Mahakama kuu iliamua kubadilisha adhabu kutoka miaka minne hadi mitano wakati
mtuhumiwa alikuwa ameomba apunguziwe adhabu.
Hivyo ni muhimu kutambua kuwa kuna
kanuni ambazo mahakama lazima izingatie katika kutoa adhabu, na kanuni hizi
zime ainishwa na sheria mbalimbali zinazotaja makosa hayo pamoja na kesi
zilizokwisha amuliwa.
[1] The
Minimum Sentence Act, Cap, 90, R.E. 2002
[2] R.
V. Kidato Abdullah 1973 L.R.T. 82
[3] R.
v . Asia Salum and Others 1986 T.L.R. 12
[4] R.
v. Kabula Mhoja, 1986 T.L.R. 248
0 comments:
Post a Comment